Habari

DKT TIZEBA AITAKA NFRA KUONGEZA JUHUDI UTOAJI ELIMU KWA WAKULIMA JUU YA UTUNZAJI WA NAFAKA

DKT TIZEBA AITAKA NFRA KUONGEZA JUHUDI UTOAJI ELIMU KWA WAKULIMA JUU YA UTUNZAJI WA NAFAKA
Sep, 11 2018

Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba (Mb) ameupongeza Uongozi wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA kwa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa (Silos) katika maeneo nane ya kanda saba za wakala ambapo ujenzi huo utaongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kutoka Tani 251,000 za sasa hadi Tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Mradi huo wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi umeanza kujengwa katika mkoa wa Dodoma, Mpanda (Katavi), Songea (Ruvuma), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga Mjini (Shinyanga), na Babati (Manyara) ambapo Serikali ya Tanzania na Serikali ya Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.

Katika hatua nyingine Waziri huyo ametoa rai kwa Mtendaji wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Bi Vumilia L. Zikankuba kuweka msisitizo zaidi katika utoaji elimu kwa wakulima kuhusu njia bora za kuhifadhi mahindi ili wakati wanapotafuta soko waweze kupata soko imara na tija kutokana na nafaka hiyo.

Mgeni rasmi Mhe Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba ametoa maelekezo hayo wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza wakati kwenye hafla ya uzinduzi wa madhimisho ya siku sikukuu ya wakulima Nanenane katika Viwanja vya Nyakabindi.

Alisema kuwa wataalamu mbalimbali wa NFRA wanapaswa kuwa Simiyu ili kutoa elimu kwa kina juu ya njia bora za utunzaji wa nafaka ya mahindi kwani kufanya hivyo kutaongeza ufahamu wa njia bora na kisasa za uhifadhi wa mahindi baada ya kuvuna.

Utekelezaji wa mikataba kati ya NFRA na wakandarasi ulianza Desemba 2017 ambapo muda wa utekelezaji ni miezi 18 tangu tarehe rasmi ya kuanza utekelezaji wa mikataba ya wakandarasi, hivyo kabla ya 2020 utakuwa umekamilika.

Mikataba ya ujenzi ilianza kufanya kazi tarehe 9 Disemba 2017 ambapo Mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) ambapo msimamizi wa utekelezaji wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kuhusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa pamoja na ukarabati wa ofisi.

Aliongeza kuwa NFRA kueleza namna ya mafanikio ya mradi huo wa maghala na vihenge vya kisasa pekee haitoshi bali inaposwa kutolewa elimu yenye msisitizo mkubwa kuhusu utunzaji wa nafaka ya mahindi.

Maadhimisho ya maonesho ya 25 ya wakulima Nanenane mwaka 2018 Kanda ya Mashariki yamefanyika Kitaifa katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoa Simiyu kwa ushirikiano wa mikoa mitatu ya Shinyanga, Simiyu na Mara.