Wakala Wa Taifa Wa Hifadhi Ya Chakula

Matukio

29 May 2016

Maafisa ubora na watunza stoo watashiriki mafunzo ya kuwaweka tayari kwaajiri ya msimu unaokuja wa ununuzi wa chakula.

Kanda ya Dodoma yasambaza zaidi ya tani elfu 2 kwa ajili ya kukabiliana na mfumuko wa bei ya chakula

Kaimu Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA - Kanda ya Dodoma) Bwana Felix Ndunguru amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi iliagiza kuanza mara moja zoezi la kuuza mahindi kiasi cha tani 2000 katika Mkoa wa Dodoma na Singida lengo likiwa ni kupunguza makali ya bei ya chakula kwa watu wa mikoa hiyo.

Bwana Ndunguru ameongeza kuwa zoezi hilo lilianza rasmi tarehe 16 mwezi Mei na limekamilika rasmi tarehe 17 Juni na kwamba sehemu kubwa ya chakula hicho kimenunuliwa na wananchi wengi na kufanilisha lengo la kupunguza makali ya bei katika mikoa hiyo.

Meneja Ndunguru ameongeza kuwa ni Halmashauri mbili ambazo hali ya ununuzi wa mahindi hayo ilikuwa ni kidogo kutokana na kuwa wananchi wengi wa maeneo hayo wapo kwenye mavuno. Amezitaja Wilaya hizo ni Manyoni na Itigi katika Mkoa wa Singida.

Akizungumzia hali hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Manyoni, Bibi Rahabu Mwagisa amesema, kwa sasa wananchi wengi wamenunua chakula cha bei nafuu zaidi kutoka kwa wafanyabiashara kwa sababu huu ni wakati wa mavuno lakini ameiomba Serikali kupitia NFRA kurejea zoezi hilo baadae mwezi Septemba, ambapo upungufu unaweza kujitokeza.

Bibi Mwagisa amesema licha ya chakula kupatikana kwa bei nafuu kwa wakati huu, kutokana na hali ya mavuno yanayoendelea, mavuno hayo si ya kuridhisha na hasa ikizingatiwa kuwa uzalishaji hukuwa wa kulidhisha katika msimu wa kilimo wa 2016/2017.

“Napenda kuiomba Serikali, kutuletea chakula cha bei nafuu, kuanzia Mwezi Septemba kwani kuna dalili, kutakuwa upungufu kwa sababu ya uzalishaji wetu kuwa mdogo” Amesema Bibi Mwagisa.

“Aidha, napenda kuwaomba wananchi kutunza chakula walichokipata, na naomba wapunguze matumizi ya chakula katika shughuli za upikaji wa pombe, hususan kwenye sherehe za jando (tohara) na unyago” Alimalizia Bibi Mwagisa.

Wilaya ya Chamwino

Akiongelea hali hiyo katika Wilaya ya Chamwino, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Chamwino, Bwana Godfrey Mnyamale amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa sababu wananchi walikuwa wakinunua kiasi cha debe la mahindi kutoka kwa wafanyabiashara wa kawaida kwa kati ya shilingi 28,000 mpka 30,000 na kuongeza kuwa mahindi kutoka NFRA yalikuwa yakiuzwa kwa kilo moja, shilingi 700 na kwa Tarafa za ndani kabisa yalifika kiasi cha shilingi 750 ambapo bei ya debe lilishuka na kufikia shilingi 12,600 na 13,500.

Bwana Godfrey amesema kwa mwaka 2016/2017 hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula haikuwa nzuri kutokana na mvua kunyesha kidogo katika Wilaya na kuongeza kuwa mahindi hayo yamesaidia kupunguza makali ya bei na kuiomba Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Dodoma kuiongezea Wilaya hiyo kiasi cha tani 300 zaidi.

“Tumeshamwandikia Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Dodoma kuhusu ombi hilo na tunaamini baada ya zoezi hili kukamilika, tutaongezewa kiasi hicho cha chakula ili kiwasaidie wakazi wa Wilaya ya Chamwino hususan watu wa Tarafa ya Chilonwa.

Wilaya ya Bahi

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Bibi Elizabeth Kitundu amesema ugawaji wa mahindi ya bei nafuu kwa wakazi wa Wilaya ya Bahi umekuwa na tija na umekuja katika wakati muhafaka.

Bibi Kitundu aliongeza kuwa Wilaya yake imepokea mahindi hayo kwa mikono miwili kwa sababu ya uzalishaji wa mtama na uwele katika msimu wa kilimo uliopita haukuwa mzuri na kwamba ni faraja kwa wananchi wa Wilaya ya Bahi.

“Tunapenda kuishukuru Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Dodoma, Wilaya yetu imekuwa ikikabiliwa na mtawanyiko wa mvua usioridhisha na hali hiyo usababisha uzalishaji wa mazao ya chakula kuwa chini.” Amekaririwa Bibi Kitundu.

Ameongeza kuwa awali mahindi yalikuwa yakiuzwa kuanzia shilingi 20,000 mpaka shilingi 25,000 kwa debe la kilo 18 wakati mahindi ya NFRA yameshuka bei mpaka kufikia debe la kilo 18 linauzwa shilingi 12,960 mpaka shilingi 14,400.

Ameongeza kuwa Kata 22 katika Wilaya ya Bahi zimepata mgao huo wa tani 400 za mahindi hayo na kuongeza kuwa kiasi kilichobaki ambacho bado hakijanunuliwa kilikuwa ni kidogona kuahidi kuwa, zoezi likikamilika watafaham kiasi gani kitakuwa kimebaki.

 

Copyright © National Food Reserve Agency 2014. All Rights Reserved