Wakala Wa Taifa Wa Hifadhi Ya Chakula

Matukio

29 May 2016

Maafisa ubora na watunza stoo watashiriki mafunzo ya kuwaweka tayari kwaajiri ya msimu unaokuja wa ununuzi wa chakula.

Kanda ya Makambako

Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Makambako yanunua Mahindi zaidi ya tani elfu 16 katika msimu wa kilimo wa 2016/2017

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Makambako Bwana Bright Mollel akimuonyesha sehemu ya shehena ya mahindi kwenye maghala ya Makambako, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara (NFRA, Makao Makuu) Bwana Joseph Ogonga, hivi karibuni.

 

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Makambako, Bwana Bright Mollel amesema Kanda ya Makambako imefanikiwa kununua shehena ya mahindi zaidi ya tani elfu 16, akiongea mbele ya wanahabari, hivi karibuni wakati wa mahojiano maalum ofisini kwake.

Bwana Mollel amesema Kanda ya Makambako ilikuwa na lengo la kununua mahindi kiasi cha tani elfu 20 katika Mkoa wa Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe ambapo katika utekelezaji wa agizo hilo, kwenye msimu wa kilimo wa 2016/2017. Wakala Kanda ya Makambako imefanikiwa kununua kiasi cha tani 16,279.298 ambapo ni sawa na asilimia 81.2 ya lengo.

Bwana Mollel aliongeza kuwa kiasi kikubwa cha shehena ya mahindi kilinunuliwa kutoka katika Mkoa wa Njombe ambapo tani 10,478,696 zilinunuliwa na kuongeza kuwa Vituo vya ununuzi vya Shaurimoyo na Mlangali vilivyo katika Wilaya ya Ludewa viliongoza kwa ununuzi wa tani 3,268.441 na tani 2167.537 za mahindi kutoka katika kila Kituo.

Kwa upande wa Mkoa wa Songwe Kituo cha ununuzi cha Ileje kilichopo Wilaya ya Ileje na kile cha Ndalambo kilicho katika Wilaya ya Momba viliongoza kwa kuwa na shehena kubwa ya mahindi ambapo kiasi cha mahindi tani 1,346.379 na tani 829.792 zilinunuliwa na Wakala.

Bwana Mollel aliongeza kuwa Kanda ya Makambako ipo katika hatua ya mwisho ya kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi mazao kabla ya msimu mpya wa ununuzi haujanza na ameongeza kuwa kwa kutumia sehemu ya fedha za ndani, Kanda imeanza kujenga ghala lenye uwezo wa kuhifadhi shehena ya mazao kiasi cha tani 5,000 na kuongeza kuwa ujenzi unatarajiwa kukamilika kabla ya msiku ujao wa ununuzi kuanza.

Bwana Mollel aliongeza kuwa ujenzi wa ghala hilo umeanza katika kiwanja kilichopo ndani ya maghala ya Mbozi katika Mkoa wa Songwe.

Aidha, Bwana Mollel alikaririwa akisema “lengo la Serikali ni kuhakikisha taifa linajitosheleza kwa chakula na ikiwezekana, Tanzania iwe ghala la chakula katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi shehena kubwa ya chakula, tutawahakikishia wakulima wa Tanzania kununua mazao yao na kuwa na ziada ya kutosha”.

Bwana Mollel aliongeza kuwa Kanda ya Makambako itafanikiwa mara dufu kuongeza uwezo wa kuhifadhi shehena kubwa ya chakula mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa maghala makubwa (silos) ambapo kwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Poland, ambapo Mkandarasi kutoka nchini Poland ameshapatikana na ujenzi unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa.

Bwana Mollel alidokeza kuwa ujenzi huo wa maghala makubwa na ya kisasa (silos) utakapokamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi wa Wakala Kanda ya Makambako mara dufu kutoka uwezo wa sasa.
Wakulima katika Kanda ya Makambako waagizwa kuzingatia ubora na kuongeza thamani ya mazao yao

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Makambako Bwana Bright Mollel akionyesha sehemu ambayo ujenzi wa ghala la chakula litakapojengwa huko Mbozi, Mkoani Songwe, kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara (NFRA, Makao Makuu) Bwana Joseph Ogonga, na wengine ni Watumishi wa Kituo cha Mbozi.

 

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Makambako Bwana Bright Mollel alitoa ushauri huo kwa wakulima wa Nyanda za Juu Kusini wakati wa mahojiano maalum.

Bwana Mollel aliwataka wakulima kuzingatia ubora wa mazao yao kama wanataka kuendelea kulima kwa faida ili baadae iwe rahisi kwao kuuza mazao yao kama mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula au wanunuzi wengine.

Bwana Mollel amesema Wakala Kanda ya Makambako imekuwa ikiwaelimisha wakulima kuzingatia ubora wa mazao yao hususan mahindi ili kuwasaidia yasikataliwe wakati wa msimu wa ununuzi unapoanza.

Bwana Mollel ameongeza kuwa Wakala imepewa dhamana na Serikali kununua mazao hususan mahindi hasa kwenye maeneo yenye ziada ya kutosha katika msimu wa mavuno lakini changamoto bado ipo kwenye ubora wa mazao.

“Naomba ikumbukwe na ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ununua mahindi kulingana na ubora wa bidhaa na kwamba mazao yanayonunuliwa na Wakala ni yale yenye kukidhi vigezo na lazima utaratibu huo tuusimamie” Amekaririwa Bwana Mollel.

Akiongelea hali hiyo, Msimamizi wa maghala ya Mbozi, Kituo kilichochini ya Wakala Kanda ya Makambako Bwana Elias Nicolaus alisema wakati wa msimu wa ununuzi unapofunguliwa mkulima anapoleta mahindi yake kwenye kituo cha ununuzi, atawakuta Watumishi wa Wakala ambao wamegawanyika kimamadaraka lakini kuna kuwa na mtu maalum ambaye kazi yake ni kuangalia ubora wa mahindi na usafi ukiwemo, na kama mahindi yanakuwa hayajafikia vigezo, uwa hayapokelewi.

BwanaElias Nicolaus ameongeza kuwa changamoto hiyo ipo kwenye maeneo machache husuan kwenye Wilaya ya Ileje na kuongeza kuwa wameendelea kuwaelimisha wakulima kuzingatia ubora wa bidhaa kabla ya kuileta kwa  Wakala.

Tunaendelea kuwaelimisha wakulima na kuwafanya marafiki ili wawe na mazoea ya kupenda kutoa mazao bora na kwamba ukiwafanya wakulima kuwa marafiki mapema, unawasaidia kwanza kupenda kuzalisha kitu bora na kizuri lakini pia kuiona Taasisi (Wakala) kama sehemu yao”. Amekaririwa Bwana Elias Nicolaus.

Bwana Elias alitoa wito kwa wakulima kulima kwa lengo la kuzalisha bidhaa itakayouzika sokoni lakini pia amewaomba wafanyabiashara na wao kuhakikisha wananunua mazao kutoka tu kwa wale wakulima walizingatia vigezo vya ubora na usafi.

“Natoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wananunua mazao kwa kuzingatia ubora wa bidhaa na usafi lakini pia azma hii njema ya Serikali itafikiwa ikiwa tutaanzisha Mamlaka ya kudhibiti ubora kama ilivyokuwa kwenye Sekta ya Mafuta baada ya Mamlaka yenye Kudhibiti na Kusimamia Mafuta (EWURA) ilipoanzishwa”. Amekaririwa Bwana Elias Nicolaus. 

Kanda ya Makambako imekuwa ikihudumia Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe na jukumu lake kubwa ni kununua chakula cha ziada katika maeneo yaliyozalisha ziada kubwa na baadae kukihifadhi kwa ajili ya kusaidia wakati wa uhitaji. Katika msimu wa ununuzi wa 2016/2017 Kanda ya Makambako ilinunua kiasi cha tani elfu 16,279.298 za mahindi na kuyahifadhi kwenye maghala.

   

Copyright © National Food Reserve Agency 2014. All Rights Reserved